Sunday, July 11, 2010

Wenger amsalandia Ngasa


NYOTA njema imeanza kumuelekea mchezaji mahiri nchini Mrisho Ngasa, baada ya Kocha Mkuu wa Arsenal ya England, Arsene Wenger kueleza kuwa amekunwa na kipaji chake.

Wenger alimuona Ngasa Jumatatu kupitia televisheni katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya timu ya Taifa ya Brazil na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kulingana na taarifa ya mtandao wa KickOff.com wa Afrika Kusini, kiwango cha Ngasa ambaye msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara alichezea Yanga na sasa amesaini Azam ambayo pia inashiriki ligi hiyo ni cha juu na atatafuta taarifa zake zaidi.

“Afrika ni mgodi wa dhahabu katika soka na kipaji kinasubiri kuibuliwa, usiku uliopita (Jumatatu), nilitazama mchezo baina ya Brazil na Tanzania.

“Tanzania walifungwa mabao mengi, lakini kulikuwa na wachezaji wawili ambao niliwaona, mmoja ni mfano wa aina ya uchezaji wa Walcott (Theo), ambaye alinifanya niseme mara moja kuwa, ninahitaji kujua zaidi, habari zake ,” alikaririwa Wenger.

Hata hivyo kocha huyo hakumtaja kwa jina Ngasa ambaye mwaka jana alienda kufanya majaribio timu ya West Ham inayoshiriki Ligi Kuu England na kukwama, lakini Ngasa ndiye anayecheza kama Walcott.

Kocha huyo mwenye sera ya wachezaji vijana, aliweka wazi kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa timu ya Taifa ya Brazil.

“Inawezekana ikatokea Brazil wakashinda michuano hii, lakini hawana vipaji vya ubunifu kama vile ambavyo walikuwa navyo kikosi chao kilichopita na hilo ndilo linanifanya nifikirie kuwa watakuwa na wakati mgumu katika michuano hii,” alisema.

Wenger anaamini kikosi cha timu ya Ivory Coast ‘The Elephants’ ndicho pekee cha Afrika ambacho kinaweza kupambana na kuleta ushindani katika kuwania Kombe la Dunia katika michuano inayoanza kutimua vumbi leo nchini Afrika Kusini.

Akizungumza kwenye hafla ya Castrol Index iliyofanyika Sandton, Afrika Kusini na kunukuliwa na mtandao huo, kocha huyo Mfaransa alisema anaamini kuwa Ivory Coast ina kikosi imara ambacho kinaweza kutoa upinzani kwa miamba wengine wa soka bila ama ikiwa na nyota wake Didier Drogba.

“Endapo Didier Drogba hatokuwa fiti, bado Ivory Coast ina wachezaji bora na kwenye suala la ushambuliaji hawajapungukiwa,” Wenger aliuambia mtandao huo.

“Endapo unataka kutazama kuhusiana na viwango vya timu, unatakiwa kutazama ni wachezaji wangapi wanacheza kwenye klabu kubwa na pengine kuna klabu kubwa kumi duniani na wana asilimia kubwa ya wachezaji katika klabu kubwa hizo kwa hiyo wana uwezo mkubwa, ingawa wako kwenye kundi gumu.

“Timu ya pili ambayo naiona inaweza kuleta ushindani ni Cameroon, wana wachezaji wazuri lakini inaonekana hawajajiandaa vyema katika maandalizi yao kwa ajili ya michuano hii.

“Kwa ujumla sina hakika kama hawana matatizo ya ndani, ambayo yanawatatiza hali inayosababisha hali hiyo,” alisema.
Wenger pia anaamini Bafana Bafana inaweza kucheza katika raundi za mwisho za michuano hiyo.

“ Swali ni kwamba Afrika Kusini ina timu nzuri ambayo imefanya katika mechi zake za maandalizi, lakini inaonekana kidogo inakosa viwango.”

Alipoulizwa ni mchezaji yupi anaamini ataibuka kuwa nyota mpya wa Afrika, Wenger alijibu kuwa: “Sijui jibu la swali hilo na kwa sasa hakuna mtu huyo, lakini katika michuano hii ya Kombe la Dunia itakuwa ni nafasi nzuri na kubwa ya kuona nani atakuwa nyota mpya wa Afrika."

Alipoulizwa kuhusiana na timu zipi anadhani zitafuzu kucheza kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia, alizitaja timu hizo kuwa ni Hispania , Argentina, England na Uholanzi.


No comments:

Post a Comment