Thursday, July 15, 2010

Anayemtaka Boban atapaswa kulipa 80Milioni


Habari kwa hisani ya Habari leo
KAMPUNI ya wakala wa wachezaji ya Ndumbaro Soccer Agency ambayo ilifanikisha mchezaji Haruna Moshi ‘Boban’ kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Sweden imesema kiungo mshambuliaji huyo amepotoka kuamua kuvunja mkataba wake na klabu ya Gefle IF na kurejea nchini.

Wakala wa mchezaji huyo anayetambulika na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Damas Ndumbaro amesema kutokana na kupotoka huko kiungo huyo amekosa nafasi ya kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza michuano ya Ligi ya Ulaya, ambayo klabu hiyo imefuzu kucheza.

Ndumbaro alibainisha hayo jana wakati akitoa ufafanuzi kuhusiana na kurejea nchini kwa Boban baada ya mchezaji huyo kuripotiwa na vyombo vya habari akidai aliamua kuachana na timu hiyo ya Sweden kutokana na maslahi madogo, ubabaishaji na kudhulumiwa fedha.

Boban alivunja mkataba na klabu hiyo Julai 4 mwaka huu na kurejea nyumbani akidai anataka kuichezea klabua yake ya zamani ya Simba, ingawa jana aliripotiwa akisema bado hadi sasa hajapata timu ya kuichezea.

Kwa mujibu wa Ndumbaro, Boban alikuwa anapata malipo yake yote ambayo ni krona 40,000 ambazo ni sawa na dola za Marekani 5,000 kwa mwezi na alipatiwa nyumba yenye samani ndani alichotakiwa ni kulipa kodi ya mwezi.

Pia alisema alikuwa akipata maslahi mengine kama kulipwa posho ya dola 200 kila anapocheza mechi, lakini asipocheza mechi kwa sababu binafsi hukatwa sehemu ya mshahara wake.

“Mbali na hayo alikuwa apewe tiketi mbili za ndege za kusafiria kwenda na kurudi wakati wa likizo na zaidi ya hayo fedha za mshahara ambazo alikuwa anakatwa kodi kwa mujibu wa sheria za Sweden angerudishiwa pindi mkataba wake unapomalizika na kutokana na yeye kuvunja mkataba huo fedha hizo sasa zinafanyiwa utaratibu ili aweze kupewa,” alisema Ndumbaro.

Ndumbaro alibainisha kuwa Aprili mwaka huu alipokea taarifa kuwa Boban ameomba kuvunja mkataba, baada ya kutokubaliana na Klabu ya Gefle IF kuhusiana na matakwa yake ya kutaka mshahara wake usikatwe kodi.

Boban aliyesaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Gefle IF kwa uhamisho wa dola za Marekani 55,000 aliyerejea nchini hivi karibuni akitokea Sweden na kudai hivi sasa ni mchezaji huru, jambo ambalo wakala wake ameamua kulitolea ufafanuzi na kubainisha kuwa hayuko huru na klabu ambayo itataka kumsajili itahitajika kumlipa wakala.

“ Kutokana na mkataba uliopo klabu ya Gefle IF inatakiwa ilipwe dola 55,000 ambazo ni sawa Sh milioni 82 za Kitanzania na Ndumbaro Soccer Agency wanatakiwa walipwe asilimia 10 ya kiasi hicho cha fedha ambacho Gefle walitoa kama ada ya uhamisho wa Boban,” alisema Ndumbaro.

Aidha Ndumbaro alisema wao wanapenda kumwona Boban akiendelea kucheza soka na klabu ambazo zinamhitaji zinatakiwa kutambua makubaliano ambayo yalitiwa saini na mchezaji huyo wakati akienda kucheza Gefle IF.

Lakini alipoulizwa jana kuhusiana na suala hilo, Boban alisema yeye hafuati heshima badala yake anafuata fedha na ndicho anachojali. “Kuwa wa kwanza maana yake nini, mimi naangalia maslahi ninayoyapata, siangalii mambo mengine. “Nahitaji fedha, hayo masuala ya heshima hayanihusu,” alisema Boban.

Hata hivyo alipoulizwa kuhusiana na madai mengine ikiwemo kutaka apewe fedha zinazotokana na viingilio, mchezaji huyo alisema hakuwa tayari kuzungumzia jambo hilo.

“Kwa sasa siwezi kuzungumzia, kama wakala anazungumza muache azungumze, kwani mtu hakatazwi kusema,” alisema Boban na kuomba atafutwe baadaye kwa ufafanuzi zaidi, ambapo alipotafutwa baadaye simu yake ilikuwa imezimwa.

Naye Clecence Kunambi anaripoti kuwa, wachezaji Thomas Ulimwengu na Yusuf Saidi walioenda nchini Sweden kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika Klabu ya daraja la kwanza ya Dalkurd FF wamefuzu majaribio yao.

Kabla ya kwenda Sweden Ulimwengu alikuwa mchezaji wa kituo cha michezo cha Tanzania Soccer Academy, ambapo pia aliongezwa kwenye kikosi cha timu ya Moro United, wakati Yusuf Said alionekana katika mashindano ya Copa Coca-Cola akiwa na timu ya Kigoma.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Ndumbaro alisema wachezaji hao wote walifanikiwa kupita katika majaribio yao na sasa wapo katika mazungumzo ya kusaini mkataba na klabu hiyo.

Alisema anajivunia rekodi ya wachezaji anaowapeleka nje kucheza soka kufuzu katika majaribio yao. Aliwataja wachezaji hao kuwa ni Boban, Joseph Kaniki ambaye baadaye alishindwa kuchezea timu hiyo kutokana na kuwa na mkataba na klabu ya Rayon ya Rwanda na Jerry Tegete ambaye hata hivyo Yanga ilimzuia kwenda.

No comments:

Post a Comment