Thursday, July 29, 2010

Azam FC JKT Ruvu Ruvu sare ya 1-1, kucheza na Simba usiku kesho Amaan Stadium





Zikicheza soka la kuvutia wakati wote wa mchezo, timu za Azam FC na JKT Ruvu zimetoshana nguvu kwa kufungana goli 1-1 katika mchezo wa kuvutia wa kirafiki uliochezwa kwenye dimba lililokarabatiwa wa Amaan visiwani Zanzibar.

Azam FC ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata goli katika dakika ya 25 lililofungwa na Ibrahim Mwaipopo kwa njia ya penati baada ya beki wa JKT Ruvu Stephano Nkomola kuunawa mpira katika eneo la hatari

Bao la JKT Ruvu lilifungwa katika dakika ya 85 baada ya mchezaji mpya wa JKT Ruvu Pius Kisambale kuukwamisha wavuni mpira wa krosi toka wingi wa kulia.

Katika mchezo wa leo, mchezaji Kalimangonga Ongala ambaye aliingia kipindi cha pili alikonga nyoyo za mashabiki kutokana na kuonesha soka la hali ya juu. Kaly alikuwa fundi sana wa kuuficha mpira, alikuwa na nguvu sana za kupambana lakini zaidi ya yote alikuwa na spidi ya kutosha na ameonesha matumaini makubwa sana.

Mchezaji Mrisho Ngasa kama kawaida yake aling’ara sana uwanjani akicheza kwa kiwango chake cha siku zote. Licha ya kupoteza nafasi mbili tatu za kufunga Ngasa alikuwa hatari muda wote wa mchezo.

Ibrahim Mwaipopo ambaye ameonekana kuongezeka misuli na spidi leo amecheza soka la hali ya juu sana, mwaipopo ana sifa iliyojificha nayo ni uwezo wa kuutuma mpira umbali mrefu na mpira ukafika pahala alipokusudia, leo ndicho kitu alichukuwa akikifanya Ibrahim, alikuwa akipiga pasi ndefu kulia na kushoto na zilikuwa zikifika barabara, penati yake aliifunga kwa ufundi mkubwa sana ambapo mpira ulianza kugonga mwamba wa juu kabla ya kutinga nyavuni. inaonekana kama licha ya kuja nyota kibao wa sehemu ya kiungo lakini nyota huyo wa Tanzania anaelekea kuilinda nafasi yake vizuri.

Tuseme nini kuhusu Jabir Aziz? Kama kuna mchezaji ambaye Azam FC imelamba dume kwenye usajili basi ni chipukizi huyu. Kwa wanaofuatilia soka la kimataifa na wanaomjua vizuri Xavi Harnandes wa FC Barcelona basi kwa huku bongo jabir ni photocopy na Xavi, Jabir leo alikuwa kila sehemu uwanjani akimiliki mipira na kuisambaza kwa wahusika utadhani mashine. Ama hakika atakaporudi Salum Abubakar toka timu ya Taifa ya Vijana Azam FC itatisha sehemu ya katikati.

Leo kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha Azam FC tumeshuhudia mapacha wawili sehemu ya ulinzi, Ibrahim shikanda upande wa kulia na Patrick Mafisango upande wa kushoto. Nawaita mapacha kutokana na aina ya uchezaji wau kwa lugha ya kiingereza ningeweza kuwaita stylish players. Kama ilivyo Shikanda, Mafisango alikuwa akicheza kwa nidhamu na ufundi mkubwa sana, anakaba kwa kutumia akili sana, anaelekeza wenzake nini cha kufanya, ana mbinu na ujuzi wa kuwasoma wapinzani kwa haraka lakini zaidi ya yote ana kipaji cha kumiliki mpira na hawa ni wachezaji ambao hawakupoteza pasi leo uwanjani.



John Bocco Adebayor leo alikuwa burudani…. Alikuwa akimiliki mipira vizuri na kuigawa kwa wenzake lakini pia wakati alipotakiwa kupiga alipiga na kulenga goli vizuri. Bocco ambeye ndiye mfungaji bora wa Azam FC wa wakati wote akiwa na miaka 20 tuu ameonesha kuwa mazuri mengi bado hayajaiva na yanaendelea kuja toka kwa kijana huyu mrefu mwenye uwezo wa kupiga kwa miguu yote na kichwa.

Aggrey Morris na Eraso Nyoni wameonesha kuwa wao ndiyo pacha bora ya Azam FC kwa upande wa walinzi wa katikati. Aggrey ana Nguvu nyingi sana na Erasto ana akili nyingi sana. Mchanganyiko huu ni mzuri sana kwenye timu na ndicho walichokionesha uwanjani, walikuwa wakipeana majukumu vizuri sana na inaonekana kwamba msimu huu tutakuwa na kikosi bora kabisa.

Mechi nyingine ni keshokutwa ambapo Azam FC itacheza usiku na Simba SC

No comments:

Post a Comment