Sunday, June 27, 2010

Papic asema TFF ni wavurugaji


KOCHA wa Yanga, Kostadic Papic amepinga kanuni mpya ya usajili iliyotangazwa na Shirikisho la Soka la Tanzania(TFF) la kusajili wachezaji watano wa kigeni kwa kueleza kuwa kanuni hizo zinavuruga taratibu za klabu.

Kauli ya Mserbia huyo imekuja baada ya TFF kusisitiza kuwa klabu za Ligi Kuu sasa zitaruhusiwa kusajili na kuchezesha wachezaji watano wa kigeni tofauti na msimu uliopita ambapo zilisajili kumi.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu kutoka Serbia aliko mapumzikoni, Papic alisema kuwa kitendo cha TFF kutoa sheria ya wachezaji watano wa nje kusajiliwa ni kuzinyima haki klabu ambazo zimekuwa na maandalizi makubwa kwa ajili ya msimu mpya wa ligi na mashindano yanayowakabili.

"Si sahihi kabisa, ligi imeisha tangu mwezi Aprili, kwa nini basi tangu mwezi Machi kabla ya ligi kuisha wangeweka wazi kanuni hiyo ili kila klabu ijue badala ya kusubiri mpaka sasa ndio wanaweka wazi wakati klabu zimeshatumia gharama nyingi kufanya usajili wake,"alisema Papic ambaye anafahamika kama Bill Clinton, raia wa zamani wa Marekani.

Papic ambaye anatarajiwa kurejea nchini Julai 15, siku tatu kabla ya uchaguzi wa Yanga, alisema, "TFF haitendi haki kwa klabu, wachezaji na sisi makocha, hichi kitu wanachokifanya hakuna sehemu yoyote duniani kinafanywa si sahihi na si haki."

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Wiki iliyopita TFF iliweka bayana kuwa utaratibu mpya wa usajili wa kutumia wachezaji watano ni wa kimataifa kwa msimu mpya utakaoanza Agosti 21 badala ya 10 kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Kanuni hiyo mpya ya TFF inatoa ahueni kwa wachezaji wa ndani, lakini ni mwiba mchungu kwa klabu za Yanga na Simba ambazo zimesheheni wachezaji wa kigeni.

Mpaka sasa ina wachezaji wanne ambao ni Yaw Berko, John Njoroge, Wisdom Ndlovu na Robert Jama Mba(ambaye ametimuliwa) na kocha wao Papic anatarajiwa kutua nchini na wachezaji wengine watatu ambao ni Kenneth Asamoah, Ernest Boakye, na Isaac Boakye, raia wa Ghana na kufikisha idadi ya wachezaji saba.

Kufuatia kanuni hiyo Yanga italazimika kuwaacha wachezaji wawili wa kigeni ili kwenda sambamba na kanuni hiyo ya TFF.

Kwa upande wa Simba, inao Joseph Owino, Hillary Echesa, Jerry Santo, Mike Barasa, Emmanuel Okwi na Patrick Ochan ambaye ni kiungo, raia wa Uganda na hivyo kulazimika kumwacha mchezaji mmoja kati ya hao.

No comments:

Post a Comment